Dodoma, Tanzania — Tasnia ya burudani nchini imepigwa na simanzi kufuatia taarifa za kifo cha msanii wa vichekesho na MC maarufu, Emmanuel Mathias, anayefahamika zaidi kama MC Pilipili, aliyefariki dunia leo Novemba 16, 2025.
Taarifa za awali kutoka kwa watu wake wa karibu zimeithibitishia OriginalEast Blog kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.
Familia Yadai Aliteswa Kabla ya Kifo
Katika mahojiano maalum, Paschal Maingu, msemaji wa familia ya marehemu MC Pilipili, ametoa taarifa nzito kuhusu mazingira ya kifo cha msanii huyo. Kwa mujibu wa Paschal, ndugu wa karibu walimweleza kuwa mwili wa marehemu umekutwa na majeraha, ishara kwamba alipitia mateso kabla ya umauti kumkuta.
“Mdogo wao wa mwisho aliniambia kapata mateso kabla hajafariki, ndio maana mpaka sasa hivi hatuna ratiba yoyote kwa ajili ya kumuhifadhi ndugu yetu. Wakirudi waliokwenda polisi tutajua, lakini amechoka,” alisema Paschal Maingu.
Aidha, familia imesema bado inasubiri maelezo rasmi kutoka kwa Jeshi la Polisi kuhusu yaliyojiri kabla ya kifo hicho, na kwamba hakuna ratiba yoyote ya mazishi hadi uchunguzi ukamilike.
Msiba Mwingine Mzito kwa Tasnia ya Burudani
MC Pilipili alikuwa miongoni mwa wasanii wa vichekesho waliokuwa wakipendwa zaidi nchini, akijulikana kwa ucheshi wake wa kipekee na uwezo wa kuchekesha jukwaani kama MC katika matukio mbalimbali.
Kifo chake kimeacha maswali mengi:
-
Nini kilisababisha majeraha aliyokutwa nayo?
-
Je, kulikuwa na tukio la uhalifu lililotokea kabla ya kifo?
-
Ni hatua gani zinazochukuliwa na vyombo vya usalama?
Mashabiki, wasanii wenzake na wadau wa sanaa wameendelea kumiminika mitandaoni kutoa pole na kuonesha mshangao kuhusu taarifa hizi.
Tunafuatilia Kwa Ukaribu
OriginalEast Blog inaendelea kufuatilia taarifa zote kutoka kwa:
-
Familia ya marehemu,
-
Jeshi la Polisi,
-
Hospitali ya Mkoa wa Dodoma,
na tutakuwa tunawaletea taarifa mpya mara tu zinapopatikana.
Bwana alitoa na Bwana ametwaa.
MC Pilipili atabaki kwenye mioyo ya wengi.



